Na Stephen Jackson, KDC
Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mhe. Job Yustino Ndugai amewataka wananchi kuchangamkia fursa za Mafunzo yanayotolewa na chuo cha Ufundi Stadi VETA - Kongwa Ili kujipatia ujuzi mbalimbali utakaowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Mhe. Ndugai amesema hayo muda mfupi baada ya ibada ya Jumapili iliyofanyika katika kanisa la Anglikana la chuo cha Theolojia cha Mt. Philip's Mjini Kongwa ambapo alialikwa kama mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa Maendeleo ya Kanisa na Jamii, (Church and Community Mobilization Project - CCMP) unaotekelezwa katika vijiji (10) katika ukanda wa Hogoro na Zoissa.
Mradi huo unajihusisha na utoaji wa Elimu juu ya matumizi sahihi ya maji kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia Nchi, na kusimamiwa na Mchungaji Canon Agripa Ndatila kama mshauri Mkuu.
Akizungumzia chuo hicho Mhe. Ndugai amesema Mafunzo yanayotolewa na VETA ni muhimu na gharama yake ni nafuu ambayo kila mwananchi anaweza kuyamudu.
Ikiwa ni Sehemu ya kuadhimisha siku ya familia duniani, Katibu wa umoja wa akinamama wa kanisa la Anglikana Tanzania (UMAKI) Bi. Margareth Ndonde aliyehubiri katika ibada hiyo amewataka akinamama kutoka kwenye familia za wachungaji, kujihusisha na shughuliza kiuchumi ili kuepuka kuwa tegemezi. Aliongeza kuwa familia zenye ustawi bora ni zile yenye kushirishana mambo mbalimbali na kutunza siri.
Katika mwendelezo wa ujumbe wake, Bi. Ndonde alisisitiza familia kujenga mahusiano mema na majirani ili kuimarisha amani katika jamii.
Kwa mujibu wa Bi. Margareth Ndonde, Umoja huo kwa mara ya kwanza utajenga shule ya Sekondari yenye Kidato cha Kwanza hadi cha Sita mkoani Dodoma kupitia michango yao.
Naye Mchungaji wa Kanisa hilo Canon Agripa Ndatila alimpongeza Mhe. Ndugai kwa kauli yake ambayo amekuwa Akiitoa Sehemu mbalimbali kuwa ifikapo Mwaka 2025 ataachia kwa hiari nafasi hiyo ili kutoa fursa kwa wengine kuongoza.
Katika hafla hiyo, Mhe. Ndugai alikata utepe na kutia Saini katika bango maalumu la mradi kama ishara ya uzinduzi, kisha kukabidhi pikipiki mbili (2) aina ya Boxer kwa matumizi ya mradi ambapo awali alikabidhi vyeti kwa wanachama wapya wa Umoja wa akinamama wa kanisa hilo.
Kwa mujibu wa Risala iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi, chuo cha Mt. Philip's kinakabiliwa na changamoto ya barabara tangu kilipoazishwa Mwaka 1914 , jambo ambalo Mhe. Ndugai aneahidi kulishughulikia katika kipindi cha miaka miwili.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.