MIL 75 KUNUFAISHA KIKUNDI CHA VIJANA WAZALENDO KONGWA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari Kongwa DC
Kikundi cha Vijana Wazalendo kutoka Mamlaka ya Mji mdogo Kibaigwa Wilayani Kongwa wamekabidhiwa Magari mawili yenye thamani ya Shilingi Milioni 75 kwa ajili ya kufanya biashara ya usafirishaji ikiwa ni mkopo unaotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri 10% kwa vikundi vya Wanawake Vijana na watu wenye Ulemavu.
Akiongea wakati wa kukabidhi Magari hayo Februari 16, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka licha ya kuwapongeza vijana hao lakini amesema kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Sulunu Hassan anatamani kuona tija ya mikopo ya 10% inayotolewa ikiinua uchumi wa Wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Aidha Mhe. Mayeka amewataka vijana hao kuyatunza magari hayo vizuri kwa kufuata sheria za barabarani ili yaendelee kuwa ushuhuda kwa vijana wengine na waendelee kuwa waaminifu ili wapate nafasi ya kukopeshwa zaidi.
Akiongea katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi amesema kuwa akiwa na kamati yake ya fedha alipata nafasi ya kuwatembelea vijana hao walipochukua mkopo wao kwa mara ya kwanza kutokana na hali yao ya marejesho waliwashauri kununua gari aina ya coaster ambayo leo wameikabidhi.
Amesema kikundi hiki cha vijana ni cha mfano wa kuigwa kwani wana nia ya dhati na biashara wanayoifanya hivyo Serikali itahakikisha inawaunga mkono kwa kuendelea kuwawezesha zaidi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omari Nkullo ameeleza kuwa huu ni utekelezaji wa ahadi ya siku 100 za Mhe. Rais ambapo aliahidi kutoa Bilioni 200 kwa ajili ya makundi maalum ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu ili kuwezesha wananchi kiuchumi ambapo vijana hao wamekuwa sehemu ya wanufaika wa fedha hizo.
Aidha Nkt. Nkullo amesema kuwa kama Halmashauri haina hofu na vijana hao watano Wazalendo kwani ni kikundi cha muda mrefu ambacho kimebobea katika masuala ya biashara ya usafirishaji ambapo kwa muda mrefu wamekuwa wakikopa na kurejesha bila usumbufu.
Akiongea kwa niaba ya vijana wenzake katibu wa kikundi cha vijana wazalendo bw. Boaz Mbele amesema kikundi chao kilianza mwaka 2015 kwa kukopa Shilingi Mil 13 wakanunua gari aina ya Probox na kufanikiwa kurejesha mkopo huo kwa wakati.
Amesema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026 kinachoanzia Oktoba hadi Desemba wamefanikiwa kukopeshwa Shilingi Mil 75 na kununua magari mawili yaani Coaster pamoja na gari ndogo aina ya Wish ili kuwasaidia kuweza kurejesha mkopo kwa wakati.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.