Na. Mbonea E. Masha
Katibu tawala mkoa wa Dodoma mhe. Kaspar K. Mmuya leo tarehe 3 Septemba, 2024, amehudhuria hafla fupi ya kukutana na wazazi pamoja na wanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Msingisa Kata ya Sagara Wilaya ya Kongwa ili kuungana nao katika chakula cha mchana pamoja na kuwatakia heri katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi itakayofanyika hivi karibuni.
Bwana Kasper Mmuya ameambatana na Afisa taaluma mkoa wa Dodoma, mwalimu Justin Machela, Afisa elimu msingi wilaya ya Kongwa Mwl. Magreth Temu na Afisa tarafa ambapo kila mmoja alipata nafasi ya kuwapongeza wanafunzi wa darasa la saba kwa hatua waliyofikia na kuwaasa waendelee kusoma kwa bidii ili wafanye vizuri mitihani yao na waweze kutimiza ndoto zao.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi kwa niaba ya jumuiya ya shule ya msingi Msingisa, mwalimu mkuu alianza kwa kurejea kauli mbiu ya shule isemayo, “Hamu kubwa ya kushinda, hushinda hofu ya kushindwa, tunastawi tulikopandwa.” kugusia ujasiri waliojengewa wanafunzi kukabili changamoto zilizo mbele yao. Akiendela kusoma risala mwalimu mkuu akaongeza kuwa jamii ya shule ya Msingisa ina imani kubwa sana kuwa mwaka 2024 utakuwa ni mwaka wa maajabu kwakuwa wanatarajia kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya mitihani ya darasa la nne na la saba na kufanya shule kuwa na wastani mkubwa
Aidha mwalimu mkuu akagusia changamoto ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya shule ikiwemo baadhi ya wazazi kuwashawishi wanafunzi wao kufanya vibaya katika mitihani ya taifa ya darasa la saba na kupelekea idadi kubwa ya wanafunzi kufeli, changamoto nyingine ni baadhi ya wazazi wachache kukataa kuchanga michango ya lishe shuleni ambayo ingewafanya wanafunzi wapate chakula wakiwa shule.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingisa, ametoa shukrani zake za dhati na kumshukuru Mhe Kaspar kwa kutembelea shule hiyo na kuonyesha imani yake kuwa ugeni wa katibu tawala wa mkoa wa Dodoma katika shule hiyo, utafanyika kuwa baraka na kufanya mwaka 2024 kuwa mwaka wa mafanikio makubwa katika jamii ya shule ya msingi ya Msingisa. Mwalimu mkuu katika risala yake, ametoa shukrani zake za dhati kwa Afisa elimu wa Wilaya mwalimu Magreth Temu ambaye amekuwa akitembelea shule ya Msingisa mara kwa mara na kuwaasa na kuwashauri kwenye mambo mengi yenye manufaa kwa shule hiyo. Mwalimu mkuu hakusita kumshukuru mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kongwa Dr. Omary Nkullo kwa kuwapatia bati ambazo zimetumika katika ujenzi wa nyumba ya kisasa ambayo itatumika kama nyumba ya mwalimu itakapokamilika.
Akijibu risala, mgeni rasmi Mhe. Kaspar Mmuya alianza kwa kushukuru jumuiya yote ya shule ya msingi Msingisa kwa kuandaa hafla hiyo na kuhudhuria kwa wingi. Katiba hotuba yake, Bwana Kaspar ametumia msemo wa elimu ni ufunguo wa maisha kusisitiza umuhimu wa elimu katika kusaidia kuona fursa na kuzitumia fursa zikaleta maendeleo. Mgeni rasmi amegusia swala la wazazi kukataa kuchangia lishe shule na kuwaeleza kuwa mtoto asipokula shule inaathiri uwezo wake wa kuwa makini katika masomo na amekemea swala la wazazi kuwashawishi watoto wao wafanye vibaya kwenye mitihani yao ili wasifaulu kwenda sekondari kwani kufanya hivyo ni kutomuwezesha mtoto asome na kupata maarifa ya kutafsiri changamoto za maisha akiwa peke yake sababu watoto hao hawatakuwa na wazazi milele na kuwashawishi kufanya vibaya ni kutengeneza kizazi cha watu tegemezi ambao wengi wao watajiingiza kwenye shughuli haramu zenye kuvunja sheria ili kujipatia mahitaji yao ikiwemo wizi, unyang’anyi na mengineyo na kuleta hasara kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha Mhe. Kaspar Mmuya amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa kuhakikisha mtoto anapata elimu na ndio maana anajenga madarasa hivyo wazazi wanapaswa wamuunge mkono mheshimiwa rais kuhakikisha juhudi zake zinazaa matunda na hazikwamishwi katika ngazi ya familia. Mhe. Kaspar amemaliza hotuba yake kwa kuwatakia kila la heri wanafunzi wote wa shule ya msingi Msingisi na kusema kuwa hana shaka kuwa wanafunzi wote waliojiandikisha watafaulu mitihani yao na kuendelea na masomo yao ili kutimiza ndoto zao.
Mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba utafanyika kuanzia Jumatano ya tarehe 11 Septemba mpaka tarahe 12 Septemba 2024 ambapo shule ya msingi Msingisi ina wanafunzi 118 waliojiandikisha na wanaotarajia kufanya mtihani huo.
pichani ni Katibu tawala Mkoa wa Dodoma pamoja na Afisa elimu msingi Wilaya ya Kongwa Mwl. Magreth Temu wakipata chakula pamoja na wanafunzi na wazazi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.