DUWASA WAPANDA MITI ENEO LA CHANZO CHA MAJI KIBAIGWA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari Kongwa DC
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Dodoma (DUWASA) wamefanya zoezi la upandaji miti katika eneo la vyanzo vya maji lililopo Kitongoji cha Mbuyuni katika Mamlaka ya Mji Mdogo Kibaigwa ikiwa na lengo la utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Akiongea katika hafla ya upandaji miti hiyo Januari 29 Mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amesema kuwa chanzo cha maji huwa hakina siasa hivyo ni vyema viongozi wa siasa wakasaidia Serikali katika kupiga vita uharibifu wa Mazingira.
Mhe. Mayeka amepiga marufuku Wananchi wanaolima na kufanya shughuli yoyote ya kibinadamu katika eneo hilo la chanzo cha maji kuacha mara moja kwani chanzo cha maji kikichezewa ni fimbo itakayomchapa kila mmoja.
Nae Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji Duwasa Bi. Rahel Muhando amesema kuwa Duwasa imeendesha zoezi hilo la upandaji wa miti 4500 katika maeneo mbalimbali ya vyanzo vya maji vilivyopo Kibaigwa na Kongwa ambapo katika eneo hilo la Mbuyuni lenye ukubwa wa hekari 28 wamepanda miti 1000.
Aidha Bi. Mhando amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu Rais Muungano na Mazingira na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika kampeni ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kuendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Mpango wa Taifa ya Uhifadhi wa Mazingira kama sehemu ya uwajibikaji wa Duwasa.
Vilevile Bi Mhando ametoa wito kwa wananchi kutunza miti iliyopandwa katika vyanzo vya maji ili miti hiyo iweze kukua na kudumu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.